HOMA ya Dengue imezidi kuwa tishio
jijini Dar es Salaam, ambapo wanamuziki watano wa Bendi ya African Stars
‘Twanga Pepeta International’, wamekumbwa na ugonjwa huo, habari
zimefika katika dawati la Risasi Mchanganyiko.
Mtoa habari Hassan Rehani ambaye ni
meneja wa bendi hiyo, alizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni na
kuwataja wanamuziki hao kuwa ni Badi Bakule, Ramadhan ‘Pentagoni’,
Bakari Kasongo ‘Mandela’, Sabrina Mbetembete na Natalia Mbui.
“Nimeshitushwa sana na ugonjwa huu,
maana katika maisha yangu ugonjwa ambao nilishawahi kuona unasumbua watu
wa sehemu moja kwa wingi kiasi hiki ni Kipindupindu tu, sasa hii
dengue ni hatari,” alisema Rehani na kuongeza kuwa wanamuziki hao
walikuwa wamelazwa Hospitali ya Mwananyamala na kwamba hali zao zilikuwa
zinaendelea vizuri.
Naye mmoja wa wagonjwa hao, Rama
Pentagoni, alipozungumza na mwandishi wetu alisema anaendelea vizuri,
huku akiuelezea ugonjwa huo kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.

No comments: