Tuesday, 13 May 2014

RICHIE AIRUDISHA BONGO MOVIE KWENYE MSTARI!!

Single Mtambalike ‘Richie’.
KWAKO,
Staa wa filamu Bongo, Single Mtambalike ‘Richie’. Naamini utakuwa uko poa na mchakamchaka wa maisha unaendelea kama kawaida. Kwa mara nyingine nimekukumbuka kwa barua.
Tofauti na wakati uliopita, leo ni pongezi; ni kawaida ya Barua Nzito, hata siku moja haijawahi kumuonea mtu.
Mtu akifanya jambo zuri huambiwa bila unafiki na akikosea basi atakula za uso!
Ndiyo maisha, ingawa najua wengi hawapendi kuambiwa ukweli lakini hapa kwenye Barua Nzito, daima nitaendelea kusimamia ukweli. Kwanza chukua tano Richie!
Wewe ni mmoja kati ya wasanii wa mwanzo kabisa kuanza kukubalika kwenye tasnia hii ya filamu. Nakumbuka enzi hizo mlikuwa na kundi lenu la Nyota Ensemble, mkiwa mastaa wanne – Aisha, Bishanga, Waridi na wewe.
Baadaye waliongezeka wengine kabla ya kujigawa na kwenda Nyota Academia 2000 na kisha Kamanda Arts Group.
Enzi zenu mlikuwa mnajua maana ya sanaa. Nakumbuka kuna wakati mlikaa pembeni kwa muda. Baadaye soko la sinema lilipoanza kukubalika mkarudi.
Hakika mlirudi na ladha tofauti. Wenye lugha wanasema: Ng’ombe hazeeni maini. Mlikuja na makali ya ukweli.
Nakumbuka sinema ulizocheza na wakongwe wenzako. Baadhi yake ni Agano la Urithi, Stranger, Mahabuba, Swahiba (zote hizi ulicheza na JB na kuwashirikisha wengine).
Nimekukumbusha haya nikitaka kuweka kumbukumbu moja muhimu; zilikuwa sinema nzuri, za Kiswahili, zenye sehemu moja tu (tofauti na Part I & 2 ya sasa inayofanana kabisa na Side A & B), hadithi kali, wasanii wazuri, mazingira halisi nk.
Badaye ule ubora ulianza kushuka na hatimaye zikaanza kurundikana sinema mbovu. Hivi majuzi, zimeanza tena sinema zenye mashiko (ziko chache sana) zenye maudhui yetu halisi Watanzania.
Kati ya sinema bora za hivi karibuni ni pamoja na Mdunduko na Kigodoro lakini wikiendi iliyopita nimeona kitu chako kipya nikaona kweli umeamua kurejesha heshima Bongo Muvi.
Filamu ya Kitendawili. Hapa nitazungumza bila woga kabisa, kama kutatolewa tuzo ya sinema bora kwa mwaka 2014, nitashangaa sana kama sinema hiyo haitashinda kipengele chochote. Inastahili.
Sinema nzuri, hadithi inaeleweka, mandhari safi tena halisi.

Tumezoea kutazama sinema zilezile kila siku, za mapenzi yaleyale, zikirekodiwa Dar ilele, lakini Kitendawili imerekodiwa Upareni (siyo kwa kuigiza, ni kweli ni Upareni kwa kila kitu).
La kufurahisha zaidi ni filamu yenye sehemu moja tu, ndefu isiyochosha! Hongera kwako Richie, lakini usisahau kufikisha hongera hizi kwa Baba Hajji, Kupa, Kinyambe na wasanii wote ulioshirikiana nao, hasa Nyamizi na yule mzee aliyeigiza kama baba yako!
Hizi ndizo filamu zinazotakiwa na mashabiki wenu. Sasa usirudi nyuma kaka, anzia hapo ulipo, endelea mbele. Chukua tano nyingine.
Yuleyule,
Mkweli daima,
...............
Joseph Shaluwa

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger Templates